Rais wa Yemen leo amependekeza mji mkuu wa Saudi Arabia , Riyadh kama sehemu inayowezekana kufufua mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa pamoja na wanaharakati wa Kishia ambao wamekamata mji mkuu wa Yemen Sanaa.
Rais Abed Rabbo Mansour Hadi ametoa pendekezo hilo katika mkutano na viongozi wa kikabila kutoka jimbo la kusini la Abyan, kwa mujibu wa washiriki wawili na msaidizi wa rais ambao wamezungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwasababu hawakuwa na ruhusa ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Wamesema Hadi amependekeza makao makuu ya baraza la ushirikiano la mataifa sita ya Ghuba kama sehemu iwapo wanaharakati wa Kihuthi wataendelea kupinga kuyaondoa mazungumzo hayo kutoka Sanaa, ambao uko katika udhibiti wao tangu mwezi Septemba, na kwenda ama Aden au Taiz upande wa kusini.
Wakati huo huo Mahakama nchini Misri imesitisha uchaguzi ujao nchini humo wa bunge, kufuatia hukumu iliyotolewa hivi karibuni na mahakama kuu ya katiba ikieleza sheria zinazoendesha uchaguzi kuwa zinakwenda kinyume na katiba.
Uamuzi huo uliotolewa leo na jaji Yahia Dakrouri wa mahakama hiyo ya utawala ulitarajiwa baada ya hukumu iliyotolewa na mahakama kuu wiki iliyopita.
Kamati ya uchaguzi nchini humo baadaye itapanga tarehe nyingine kwa ajili ya uchaguzi huo. Kamati ya uchaguzi imesema inafanyia kazi kubadilisha sheria hiyo.
Uchaguzi wa bunge ulipangwa awali kufanyika kwa awamu kuanzia Machi 22, ikiwa awamu ya mwisho katika kipindi cha mpito kufuatia kuondolewa mwaka 2013 kwa rais Mohammed Mursi na jeshi.